Header Ads

RAIS MAGUFULI AWALILIA MARIA NA CONSOLATA

Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia, Masista wa Maria Consolata na wote walioguswa na kifo cha mabinti mapacha walioungana Maria na Consolata Mwakikuti waliofariki dunia jana jioni katika hospitali ya Mkoa wa Iringa.

Mhe. Rais Magufuli aliwatembelea Maria na Consolata walipokuwa wakipata matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es salaam tarehe 06 Januari, 2018.
Pamoja na kuwapa pole, Maria na Consolata waliongoza sala ya kuliombea Taifa na Viongozi wake.

Mhe. Rais Magufuli anasema anatambua kuwa Maria na Consolata walikuwa na ndoto kubwa ya kuja kulitumikia Taifa baada ya kumaliza Chuo Kikuu cha Masista wa Consolata Ruaha (RUCO) walikokuwa wakiendelea na masomo yao, lakini haikuwa hivyo.

Amewaombea Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema peponi, Amina

Tangu mwishoni mwa mwaka jana, mapacha hao walifanyiwa uchunguzi mara kadhaa baada ya kupata matatizo ya moyo.

Mapacha hao waliwahi kulazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya Matibabu wakitolewa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Iringa.

Katika safari ya elimu, Maria na Consolata walionesha uwezo mkubwa tangu walipohitimu na kufaulu Darasa la Saba mwaka 2010 katika Shule ya Msingi ya Ikonda wilayani Makete, baadaye walijiunga na Kidato cha Nne katika shule ya Sekondari ya Udzungwa iliyopo Wilayani Kilolo

Walisoma pia kidato cha 5 na 6 katika shule hiyo na baadaye walijiunga na Elimu ya Juu katika Chuo Kikuu cha Ruaha(RUCU) baada ya kupata daraja la 2 katika mtihani wa Kidato cha 6

Maria na Consolata walizaliwa katika Hospitali ya Misheni ya Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe mwaka 1996.

No comments

Powered by Blogger.