Header Ads

SHIRIKA LA PAD KUTOKA SONGEA LAPONGEZA KAZI ZA WASAIDIZI WA KISHERIA ZINAZOFANYWA NA SHIRIKA LA MAPAO WILAYANI MAKETE



Bi.Suzana Mkwele kutoka Shirika la PAD Songea akiwa katika Mkutano wa pamoja na wasaidizi wa Kisheria kutoka kata zote za Wilaya ya Makete mkoani Njombe waliokutana Ofisi za Makao makuu ya Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Wilayani hapa Kijiji cha Iwawa Makete Mjini.

Shirika la PAD kutoka Mkoani Ruvuma limepongeza shughuli za usaidizi wa Kisheria zinazofanywa na wasaidizi wa Kisheria Wilayani Makete chini ya Mkurugenzi wa MAPAO Mch.Denis Sinene.

Pongezi hizo zimetolewa hii leo na Bi.Suzana Mkwele kutoka Shirika la PAD Songea akiwa katika Mkutano wa pamoja na wasaidizi wa Kisheria kutoka kata zote za Wilaya ya Makete mkoani Njombe waliokutana Ofisi za Makao makuu ya Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Wilayani hapa Kijiji cha Iwawa Makete Mjini.

Huku akipongeza jitihada zinazofanywa na wasaidizi hao Kisheria kwa kutoa msaada wa kisheria kwa wananchi pamoja na ushirikiano Mkubwa walionao na Serikali katika kuwasaidia wananchi kutatua migogoro mbalimbali wanayokumbana nayo kwa kufuata haki.

“Nimepita vituo vyote vya Wasaidizi wa kisheria kwa kanda hii lakini sijaona mshikamano mlionao ninyi MAPAO na Serikali mko na ushirikiano mzuri sana nawapongeza mno,lakini si hivyo tu hata huduma mnayoitoa kwa wananchi wa Makete kwa kweli mnahitaji kupongezwa sana tena sana”Aliongeza Bi.Susaza Mkwele.

Wasaidizi wa Kisheria kutoka kata Mbalimbali za Wilaya ya Makete akiwemo Jaclin Mbilinyi kutoka kata ya Isapulano,Prosper Sanga maarufu kama tatizo kutoka kata ya Kinyika pamoja na Bathromeo Mahenge kutoka kata ya Iniho wamepongeza uongozi wa Shirika hilo ngazi ya Wilaya kwa kuanzisha Klabu za Wasaidizi wa Kisheria ngazi za shule za Msingi na Sekondari.

Bathromeo Mahenge Msaaidizi wa Kisheria kutoka kata ya Iniho amesema “kwanza niwapongeze viongozi wetu kwa kazi nzuri mnayoifanya lakini niombe mje hata kwetu Iniho kuna sekndari ya Mwakavuta pale lakini kuna shule nyingi tu za Msingi kwenye kata ya Iniho mje mfungue Klabu za wanafunzi’’.

Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Wilayani Makete(MAPAO) Mch.Denis Sinene amewataka wasaidizi wa kisheria kutoka kata zote kuendelea kutoa Elimu kwa wananchi huku akiwasihi kufika shule za Msingi na Sekondari kwa ajili ya kuwasaidia watoto kutambua haki zao za Msingi kupitia shirika hilo na wao kama Viongozi wataendelea kuongeza nguvu katika kutoa Elimu ya Msaada wa kisheria kwa shule mbalimbali Wilayani hapa.

Wakati huohuo Mkurugenzi wa MAPAO ametoa pongezi kwa Redio Kitulofm kwa kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu Elimu inayotolewa na wasaidizi wa Kisheria kutoka kata mbalimbali Wilayani hapa pamoja na kutoa muda wa kurusha vipindi bure kila wiki mara moja vinavyohusu Msaada wa Kisheria

Mwanasheria Halmashauri ya Wilaya ya Makete Ndg.Godfrey Gogadi ameelezea kufurahishwa kwake na huduma zinazotolewa na Shirika hilo na kuongeza kuwa kwa sasa wananchi wengi wamekuwa wakipata Msaada wa kisheria kutoka kwa wasaidizi hao na hata katika ofisi yake malalamiko na wahitaji wa Msaada wa kisheria wamepungua kwa kuwa wanapata huduma kutoka kwenye kata zao.

Pia amewasihi wasaidizi hao kujiepusha na vitendo vya Rushwa katika utoaji wa huduma ya Msaada wa Kisheria kwa wanaJamii na kufikia Lengo la kuwa na Jamii yenye haki
 Mkurugenzi wa Shirika la Wasaidizi wa Kisheria Wilayani Makete(MAPAO) Mch.Denis Sinene akielezea kazi zilizofanywa na Wasaidizi wa Kisheria kutoka kata mbaimbali Wilayani hapa

Mwanasheria Halmashauri ya Wilaya ya Makete Ndg.Godfrey Gogadi akisisitiza wasaidizi hao kujiepusha na vitendo vya Rushwa wakati wa utoaji wa haki kwa wananchi
Wasaidizi wa Kisheria kutoka kata Mbalimbali za Wilaya ya Makete wakifuatilia maada zilizokuwa zikijadiliwa kwenye Mkutano huo uliofanyika hii leo ofisi za MAPAO Makete Mjini



No comments

Powered by Blogger.