UJENZI WA BWENI MANG'OTO SEKONDARI ULIPOFIKIA NA FAINI ALIYOPEWA MZAZI WA MWANAFUNZI ALIYEUNGUZA BWENI
Ujenzi wa Bweni la Wavulana shule ya Sekondari Mang'oto Wilayani Makete Mkoani Njombe umefikia mahali pazuri baada ya wananchi wa Kata hiyo na wadau wa Maendeleo Makete kulivalia Njuga Suala hilo lililowaacha kwenye Matatizo Wanafunzi wa shule hiyo kwa kipindi cha Miezi miwili iliyopita
Hivi sasa Ujenzi wa Bweni hilo umefikia hatua ya kupiga bati ambayo tayari imekamilika ikiwa imesalia kumalizia ukamilishaji wa sakafu,rangi,dari,kufunga Milango na Madirisha pamoja na ununuzi wa Vitanda kwa ajili ya kuanza kutumika
Diwani wa kata ya Mang'oto Mh.Osmund Idawa amesema changamoto kubwa ambayo imebaki hivi sasa ni kutokuwa na fedha ya ununuzi wa Vitanda ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kulalia wanafunzi hao ambavyo vinatarajiwa kutengenezwa Vitanda vya Chuma toauti na vilivyokuwepo awali vitanda vya Mbao ambavyo viliteketea kwa moto bweni hilo lililoungwa na Mwanafunzi wa kidato cha pili
Ujenzi wa Bweni hilo umepigwa tafu kwa kiasi kikubwa na Chama cha Maendeleo Makete(MDA) ambacho kilisaidia ununuzi wa Bati 150 ambazo zimetumika kufunika paa la bweni hilo pamoja na misumari ya bati kilo 10 na Mifuko 100 ya Saruji
Nguvu kubwa za wananchi wa Kata ya Mang'oto wamezielekeza katika ujenzi wa Bweni hilo kwa kutoa tofari pamoja na fedha kwa kila mwananchi mwenye nguvu kuchangia shilingi Elfu tano,Viongozi wa Vijiji na watumishi wote wa Umma waliopo kwenye kata hiyo
Diwani wa kata ya Mang'oto Mh.Osmund Idawa amesema ujenzi wa Bweni hilo unatarajiwa kukamilika mwezi ujao na wanafunzi waanze kulitumia jengo hilo kwa kuwa sasa wanafunzi zaidi ya 100 wanalala ndani ya vyumba vya Madarasa jambo ambalo bado ni hatari kwa Afya za wanafunzi na upungufu wa vyumba vya Madarasa
Mwanafunzi Essau Msigwa alichoma bweni hilo usiku wa kuamkia tarehe 12 march 2018 na amehukumiwa kifungo cha nje cha miaka mitatu huku Baba yake Mzazi ambaye pia ni Mwalimu shule ya Msingi Makangalawe iliyopo kwenye kata hiyohiyo ya Mang'oto Aldo Msigwa akipigwa faini ya Milioni nane ambayo ameanza kupunguza ikiwa mpaka sasa ameshapunguza kiasi cha shilingi Milioni tano zilizosaidia katika ujenzi wa Bweni unaoendelea huku akiwa bado anadaiwa Milioni tatu ili kumalizia faini aliyopewa
Ujenzi wa Bweni hilo ulipofikia sasa(Picha na Award Mpandila Katibu wa Chama cha Maendeleo Makete MDA)
Wananchi wa Kata ya Mang'oto walipokuwa wakishiriki nguvu kazi katika uwekaji wa kokoto iliyochanganywa na Saruji ujenzi ulipokuwa hatua ya Linta
No comments