PICHA: Mwigulu Nchemba aongoza uchomaji moto shamba la bangi ekari sita
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ameongoza operesheni ya
kuteketeza ekari sita za bangi zilizokuwa zimelimwa katikati ya msitu
uliopo kijiji cha Engalaoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Uteketezaji huo umefanyika leo Februari 7, 2018 ambapo Mwigulu, Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Charles Mkumbo na baadhi ya askari wamelazimika kutembea kwa miguu umbali wa kilomita 2 kwenda katika msitu huo, huku wamiliki wa mashamba wakitokomea kusikojulikana.
Bangi hizo zilivunwa kutoka shambani, kurundikwa sehemu moja na kisha kuchomwa moto.
Mwigulu
amesema Serikali itaendelea na operesheni hiyo nchi nzima na haitasita
kuwakamata wahusika wote na kutaifisha magari yanayotumika kusafirisha
bangi.
Amewataka polisi kuongeza juhudi kupambana na wanaotengeneza dawa za kulevya viwandani.
Kwa
upande wake Mkumbo amesema ekari sita za mashamba ya bangi
zimeteketezwa na kusisitiza kwamba operesheni hiyo ni endelevu katika
mkoa wa Arusha na wilaya zake.
Amesema kwa sasa wanaolima bangi wamebuni mbinu ya kulima katikati ya misitu ili kukwepa kukamatwa.
“Wananchi
wanapaswa kubadilika kwa kulima mazao yenye tija badala ya bangi.
Polisi kama walinzi wa usalama hatutakubali kuona vijana wanaathirika
kwa matumizi ya dawa za kulevya,” amesema.
“Walidhani
kulima bangi katikati ya misitu hatutawabaini. Polisi tuna mbinu nyingi
na hatutakubali kuona vijana wetu wanaharibikiwa kwa sababu ya bangi.”
No comments