Dr Slaa Aeleza Sababu za Kutompa Pole Tundu Lissu
Balozi
mteule, Dk. Willibrod Slaa ameeleza sababu za kutompa pole Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi na watu
wasiojulikana Septemba 7, mwaka jana.
Dk.
Slaa ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chadema, alitoa kauli hiyo jana
wakati akihojiwa na kipindi cha 360 kinachorushwa na Kituo cha
Televisheni ya Clouds.
“Suala
la Lissu nilishachokozwa sana kwenye mitandao ya kijamii kuwa kwanini
sijatoa pole sasa mimi sioni kama pole inalazimishwa.
“Kama
binadamu hakuna anayependa mwenzake aumizwe lakini matukio ya kuumiza
yametokea mara nyingi sana nchini, sasa mimi si chombo cha dola
kunyooshea kidole mtu, sheria inasema kama kuna mtu unamhisi unaenda
polisi,” alisema.
Alipoulizwa
endapo amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe
alisema: “Nitaongea naye vipi na mwenyekiti wa chama wakati mimi
nilishaachana na siasa za vyama.”
Alipoulizwa iwapo Mbowe akimpigia atakubali kuonanana naye alisema: “Sasa itategemeana na mazingira ya kuonana.”
Akizungumzia
mwenendo wa siasa za upinzani hapa nchini, Dk. Slaa alisema
haumfurahishi kwa sababu alishiriki kujenga upinzani lakini haoni chama
chenye sera zilizonyooka.
“Mwelekeo
wa siasa za upinzani nchini haunifurahishi, baada ya uhuru mwaka 1963
kulikuwa na vyama vingi, baadaye vikaanza kufa vyenyewe kwa sababu
vilikatisha tamaa wananchi na baadaye vikaondoka kisheria.
“Sasa naona tena dalili hizo za mwaka 1963 kwa sababu hatuelekei pazuri…wanaongea juu juu lakini mikakati ya utekelezaji hakuna.
“Sioni
uimara wa vyama na mkakati wa kutupeleka mbele, wanachofanya wanasubiri
kiongozi wa serikali atoe kauli halafu wanakuja na kusema hili sio
lakini hakuna sera mbadala,” alisema Dk. Slaa.
Kuhusu
kuzuiwa mikutano ya siasa alisema hakubaliani na marufuku ya siasa kwa
kuwa Bunge ndiyo ilipitisha lakini pia hakuna hati yoyote iliyotolewa na
Rais John Magufuli kwamba mikutano ni marufuku.
“Sikubaliana
na taratibu kuwa mikutano imepigwa marufuku, lakini mara kadhaa
nimekuwa nahoji hawa wanasiasa wanionyeshe hati yoyote iliyotolewa na
rais kuwa mikutano imepigwa marufuku kwa sababu rais anafanya kazi kwa
kufuata sheria,” alisema.
No comments