Header Ads

NYUMBA YAUNGUA KWA MOTO MAKETE

 Nyumba hiyo ikionekana juu ya paa sehemu ambapo waokoaji walilazimika kubomoa Bati kwa ajili kuona juu ya dari kama bado kuna moto unaoendelea kuwaka
 Baadhi ya wananchi wakiwa nje ya Nyumba hiyo baada ya kuuzima moto huo

 Baadhi ya vitu vilivyokuwemo ndani vikionekana baada ya kutolewa nje

Na Furahisha Nundu

Matukio ya nyumba kuungua yamezidi kushamiri Mji mdogo wa Iwawa hususani Kitongoji cha Dombwela Wilayani Makete baada ya nyumba nyingine kuungua hii leo na chanzo chake kikidaiwa kuwa huenda ni Shoti ya Umeme

Tukio la kuungua kwa Nyumba ya Mwanamke mmoja Aliyetambulika kwa Jina la Agatha limesababisha Samani mbalimbali kuteketea kwa moto huo ikiwemo Sofa na vifaa vingine ambavyo bado thamani yake haijajulikana

Mama anayeishi kwenye nyumba hiyo Kitongoji cha Dombwela karibu na Msikitini ambaye hakuwepo wakati tukio hilo linatokea amesema "Nilikuwa Kanisani nimeondoka hapa nyumbani saa nne kasoro na hapakuwa na mtu ghafla nikiwa Kanisani nikaja kuambiwa nyumbani kuna tatizo nirudi lakini nafika nyumbani nakuta watu wamejaa nje ya nyumba na vyombo vyote vikiwa nje hapa".

"Sijui chanzo cha moto huu ni nini lakini kusema ni Jiko la Mkaa hapana mimi sijawahi kutumia jiko hilo natumia kuni,Lakini kwa kweli nawashukuru Majirani na watu wote waliozima moto huu Mungu awabariki sana" Alisema Agatha.

Agnes Sanga ni jirani yake na Agatha yeye alikuwa shuhuda wa kwanza kufika eneo la tukio amesema alipoona nyumba inatoa moshi alipiga simu kwa watu wengine na kuwaita majirani na kuanza kubomoa Milango na Madirisha ndipo wakaona moto unawaka ndani ya Sebule na kuanza kuuzima kwa kutumia Maji.

Ameongeza kuwa watu walikusanyika Haraka na kuanza kusaidia kuzima moto huo jambo ambalo walifanikiwa kwa kiasi fulani kuokoa mali zilizokuwemo ndani,huku akisema moto huo unaonekana ulianzia juu ya Dari Sebuleni.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Dombwela Ndg.Joseph Mbilinyi amesema kwamba anasikitishwa na tukio hilo huku akiwashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi kuuzima moto huo na kuokoa mali zilizokuwepo ndani ya nyumba hiyo

Hili ni tukio la tatu kutokea kwa kipindi cha miezi Isiyozidi mitano katika Kitongoji hicho cha Dombwela Mji mdogo wa Iwawa




No comments

Powered by Blogger.