MILIONI 39 ZIMETUMIKA UJENZI WA ZAHANATI YA KIJIJI IPEPO WILAYANI MAKETE
Mwonekano wa Zahanati hiyo kwa nje
Zaidi ya Shilingi Milioni 39 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ipepo Kata ya Ipepo Wilayani Makete Mkoani Njombe.
Katika ujenzi wa Zahanati hiyo Serikali imetoa Shilingi Milioni 20, huku Milioni 17 zikitolewa na Usharika wa Home uliopo Nchini Ujerumani kiasi kingine cha fedha ni kutoka kwa Wananchi,nguvu kazi pamoja na Wadau wa Maendeleo wazawa wanaoishi nje ya Kijiji hicho.
Kufuatia Ujenzi wa Zahanati hiyo wananchi wa Kijiji cha Ipepo wamesema uwepo wa Zahanati hiyo kwa sasa utawapunguzia adha waliyokuwa wakikumbana nayo kwa kutumia gharama nyingi kusafiri kwenda kutibiwa vijiji jirani kama Igolwa na Maliwa.
Wakizungumza katika Uzinduzi wa Zahanati hiyo Mbele ya Mganga Mkuu wa Wilaya ya Makete aliyekuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo Mwishoni mwa wiki jana Daktari ITIKIJA EDWARD MSUYA Wananchi hao wamesema "Tulikuwa tukisafiri kwa shilingi Elfu kumi mpaka elfu kumi na Tano lakini kwa sasahivi tunapata huduma hapahapa,Akina Mama wajawazito ndio waliokuwa wakipata shida kubwa sana wakihitaji Msaada wa Huduma ya Haraka".
Akizungumza katika Uzinduzi huo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Makete Daktari ITIKIJA MSUYA amesema Uwepo za Zahanati hiyo ni Mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inawafikishia Huduma bora wananchi ambayo itakuwa karibu zaidi kwa kuwajali akina Mama wajawazito na watoto
Daktari Msuya ameongeza kuwa Uongozi ngazi ya Wilaya umeshapeleka Mtoa huduma mmoja Kwenye Zahanati hiyo na itaongeza wahudumu kwa Kadri watakavyopatikana
Ujenzi wa Zahanati hiyo ulianza mwaka 2012 na kukamilika mwaka huu 2018
No comments