MWANAFUNZI WA KIKE AJIUA BAADA YA KUNASWA NA SIMU YA MPENZI WAKE
Mwanafunzi wa kidato cha pili mkoani Mtwara, Salma Abdalah aliyekuwa akiishi Mbawala Chini, amefariki dunia kwa kujinyonga, baada ya kukutwa na simu ambayo alipewa na mpenzi wake.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara Lucas Mkondya, amesema tukio hilo limetokea mwanzoni mwa wiki hii baada ya wazazi wa binti huyo kuamua kumfukuza nyumbani na kumtaka kwenda kuishi kwa bibi yake kutokana na utovu wa nidhamu, na ndipo akaamua kujitoa uhai wake.
Kamanda Mkondya ameeleza kuwa wazazi wake waligundua kuwa binti yao alikuwa akimiliki simu ambayo hawajamnunulia na walipomuuliza hakuwa na jibu sahihi, ndipo baba yake ambaye ni baba wa kufikia aliamua kumfukuza nyumbani kutokana na kuchoshwa na tabia zake za utovu wa nidhamu, na kuelekea sokoni kwenye biashara zake kumtafutia nauli, huku mama yake akielekea shambani kwenye shughuli zake za kilimo,
Taarifa zaidi kutoka kwa mashuhuda wa tukio wamesema binti huyo alipojinyonga aliacha ujumbe uliosema kwamba "Nampenda sana Daudi, siwezi kukaa naye mbali najua hili ni kosa kwangu lakini nawaomba wazazi wangu mumpende sana Daudi maana akiwa kwenye matatizo, mimi sitajisikia vizuri"
CHANZO:MALUNDE BLOG
No comments