Rais Magufuli aagiza kufungiwa kwa benki na kampuni za simu.....Aaagiza Milioni 100 Alizopewa Kama Zawadi Zikatumike Kujenga Wodi ya Wagonjwa
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, ameagiza
mamlaka husika kuzichukulia hatua ikiwamo kuzifungia kampuni za simu na
benki ambazo zitashindwa kuanza kutumia mfumo wa ukusanyaji wa mapato
kwa njia ya kielektroniki ifikapo mwisho wa mwaka huu 2017.
“Kwa
kampuni za simu au benki zitakazoshindwa kutekeleza agizo hili,
taratibu husika zifanyike. Ikiwezekana makampuni hayo au benki hizo
zifungiwe kufanya kazi nchini” amesema Rais Magufuli.
Rais
Magufuli ameyasema hayo leo mjini Dodoma katika hafla ya ufunguzi wa
tawi la benki ya CRDB lililopo katika jengo la LAPF-Dodoma.
Rais
amezitaka benki zote pamoja na makampuni ya simu ambayo yanataka
kuendelea kufanya biashara hapa nchini kuhakikisha kuwa wanajiunga na
mfumo huu wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki kabla ya
kufika mwisho wa mwaka huu wa 2017.
“Kwa
taarifa nilizo nazo ni benki chache tu ambazo tayari zimejiunga na
mfumo huu wa ukusanyaji wa mapato kwa njia ya kielektroniki. Benki na
kampuni nyingi za simu bado hazijajiunga na mfumo wa ukusanyaji wa
mapato kwa njia ya kielektroniki. Benki na Kampuni zote za simu
zinazotaka kufanya biashara Tanzania zihakikihshe zinajiunga na mfumo
huu kabla ya mwaka huu (2017) kuisha,” amesema Rais Magufuli.
Aidha
Rais Magufuli ameagiza fedha kiasi cha shilingi 100 milioni alichopewa
kama zawadi na Benki ya CRDB zitumike kujenga wodi ya wagonjwa katika
hospitali ya Dodoma na kutaka wodi hiyo iitwe ‘wodi ya CRDB’ kama ishara
ya heshima kwa benki hiyo.
Akiikabidhi
hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rais Magufuli ameonya wahusika
wote kutumia vizuri fedha hizo ili kuhakikisha ujenzi wa wodi hiyo
unakamilika kwa wakati na kwa kiwango kinachofaa.
No comments