Barabara ya UKWAMA Makete yakamilika
Muonekano wa Barabara hiyo baada ya kutengenezwa
Mkandarasi wa barabara hiyo Bw. Asajile Mbwilo
Diwani wa UKWAMA Mh Augustino Tweve
Mwananchi wa Ukwama Charles Sanga akizungumza na sisi
Hatimaye tatizo la
kushindwa kupitika kwa barabara ya Ihobwela Hadi UKWAMA kata ya Ukwama wilayani
Makete mkoani Njombe lililotokana na matengenezo ya barabara hiyo limemalizika
baada ya mkandarasi kukamilisha kazi hiyo
Awali barabara hiyo
ilipokuwa kwenye matengenezo ilipelekea adha kubwa kwa watumiaji ikiwemo
kupanda kwa gharama za usafiri hasa bodaboda kutoka shilingi 4000 kwenda na
kurudi hadi kufikia sh. 30,000 kwenda na kurudi
Blog hii imetembelea
barabara hiyo kuanzia Ihobwela hadi Ukwama zikiwa zimepita wiki mbili tangu
tutangaze kutopitika kwa barabara hiyo, na kukuta barabara hiyo inapitika kama
awali baada ya mkandarasi kusambaza na kushindilia vifusi vilivyokuwepo
barabarani hapo
Akizungumza nasi akiwa eneo la matengenezo ya barabara hiyo, Mkandarasi huyo Bw, Asajile
Mbwilo amesema matengenezo ya barabara hiyo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia
80 na barabara inapitika kama kawaida huku akiwapongeza Mkuu wa wilaya ya
Makete Mh Veronica Kessy na mwenyekiti wa halmashauri Mh Egnatio Mtawa kufika
kujionea hali ilivyokuwa awali kwenye barabara hiyo pamoja na Diwani wa kata ya
Ukwama Mh. Augustino Tweve
Amesema kwa sasa
kinachoendelea ni kufanya matengenezo ya kuzibua mitaro ili maji yapite na
yasiharibu barabara pamoja na kuweka makalavati sehemu zinazohitajika kufanya
hivyo
Pia amewaomba
wananchi kuwa na uvumilivu wakati matengenezo ya barabara hiyo yanapofanyika
kwa kuwa katika hatua za mwanzo za matengenezo hujitokeza changamoto mbalimbali
ambazo kwa haraka wananchi hudhani hakuna kinachoendelea na kuanza kutoa lawama
kumbe matengenezo yanaendelea na mwishowe ujenzi hukamilika
Diwani wa kata ya
UKWAMA Mh. Augustino Tweve amesema tatizo lililokuwepo awali kwa sasa halipo
kwa kuwa huduma zimerejea kama kawaida baada ya barabara hiyo kukamilika na
kuiomba jamii kuliona na kulitambua hilo
Pia amewaomba
wananchi kushirikiana naye kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuwa walimtuma
kuwatumikia na yeye amehakikisha anawatumikia kama walivyomtuma na ndiyo maana
ameshirikiana na viongozi mbalimbali wa halmashauri na mkandarasi kuhakikisha
barabara hiyo inapitika kama kawaida
Baadhi ya wananchi
waliozungumza na AM blog akiwemo Amasha, Charles Sanga na Agnes Ngailo wamempongeza
mkandarasi, diwani wao na serikali kwa ujumla kwa kupambana kuhakikisha
barabara hiyo inaendelea kupitika kama mwanzoni
Wamesema ni kweli walikuwa wakipata tabu mwanzoni wakati vifusi havijasambazwa, lakini sasa baada ya matengenezo kukamilika huduma zimerejea kama mwanzoni
No comments