Header Ads

DC aagiza kukamatwa kwa Wazazi wa Wanafunzi 55 waliopata ujauzito

Wakati baadhi ya viongozi wa Serikali wakieleza kuwa wanafunzi wanaopata mimba watafikishwa mahakamani, wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu wamesema hatua hiyo si suluhisho la kumaliza tatizo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara, Sebastian Waryuba ameagiza polisi wilayani humo kuwakamata wazazi na wanafunzi 55 wa sekondari waliopata ujauzito hata kama walishaacha shule miaka miwili iliyopita ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki katika kikao cha kamati ya ushauri ya wilaya baada ya kutopokea taarifa ya elimu kutoka kwa Ofisa Elimu Sekondari, Sostenes Luhende kuhusu wanafunzi hao kupata ujauzito kati ya Januari na Desemba.

“Nataka kupata taarifa za wanafunzi waliopata ujauzito ni wa shule gani, jina lake na la mzazi wake na hatua zilizochukuliwa; taarifa hizi ziletwe kwangu na nakala ziende kituo cha polisi kwa ajili ya uchunguzi ndiyo maana nimeagiza kukamatwa kwa wahusika pamoja na wazazi wao,” alisema Waryuba.

Kauli kama hiyo ilitolewa Desemba 11 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella aliyewaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri mkoani humo kuwakamata na kuwaunganisha kwenye kesi wanafunzi wa kike watakaopata ujauzito kwenye maeneo yao.

Mongella alitoa agizo hilo wakati wa kikao cha wadau wa elimu mkoani Mwanza akisema hatua hiyo licha ya kuwatia hofu ya kutojihusisha na vitendo vya ngono, pia itawezesha wanaopata ujauzito kuwataja wahusika na kutoa ushahidi mahakamani.

“Kuna tabia ya wanafunzi wanaopata ujauzito kutowataja wahusika na inapotokea wamewataja, basi hawafiki mahakamani kutoa ushahidi; sasa tuanze kuwaunganisha kwenye kesi kukomesha mimba shuleni,” alisema Mongella.

Akizungumzia hatua ya viongozi hao wa Serikali, Ofisa Miradi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Deo Temba alisema hilo si suluhisho.

Alisema wanafunzi wengi huathiriwa na mazingira magumu yanayowazunguka ikiwamo umaskini, uhaba wa mabweni, kutembea umbali mrefu na vishawishi kutoka kwa watu wanaowazunguka.

Akitoa mfano, alisema madereva wa bodaboda ni miongoni mwa makundi hatarishi kwa watoto wa kike wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule kutokana na uhaba wa mabweni.

“Fikiria mtoto wa kike hajala chakula nyumbani kwao kwa sababu hakipo, anatembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule ni namna gani atakwepa kishawishi cha bodaboda anayempa lifti kila siku? Wakati wasichana wanaagizwa kukamatwa, viongozi waone namna ya kumaliza changamoto zinazowakabili watoto wa kike,” alisema.

Alisema ni vizuri wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya mimba za utotoni kukaa na wananchi ili watafakari, wajadili na kupata suluhisho la nini cha kufanya kwa sababu kupitia mazungumzo watajua chanzo.

Kwa mtazamo wake, ofisa wa kitengo cha jinsia wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Godfrida Jola alisema kuwakamata na kuwaadhibu ni wazo linaloweza kuwafanya wengine waogope kujiingiza kwenye vitendo hivyo ikiwa mazingira ya mahabusu na magereza yataandaliwa kuwapokea watoto wajawazito.

“Japokuwa kuwakamata ni wazo zuri lenye lengo la kuwatisha, lakini wanawapeleka wapi? Kama ni magereza, kuna mazingira ya kuwawezesha wajawazito kuishi vizuri? Itafutwe njia nyingine hii si sahihi,” alisema Jola.

Mratibu wa Shirika la Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDS), Onesmo Ole Ngulumwa alisema viongozi wamekuwa wakitoa matamko yanayokinzana na sheria.

Alisema kutaka wasichana waliopata ujauzito wakamatwe wakati wakijua wengi wana umri wa chini ya miaka 18 ni kupingana na sheria zilizopo.

Alisema wasichana wanaopata ujauzito wakiwa chini ya miaka 18 kisheria wanahesabika kuwa wamebakwa.

Ole Ngurumwa alisema wasichana wa aina hiyo wamepata ujauzito bila ridhaa yao.

“Sasa unamkamata vipi na kumfungulia mashtaka msichana aliyebakwa? Unamfungulia mashtaka gani, matamko ya aina hii ni hatari,” alisema.

Alisema wanaopata mimba wakiwa na umri huo kuna mazingira mengi ambayo yanasababisha hali hiyo ingawa ni wachache ambao wanafanya vitendo hivyo kwa hiari.

“Tusitoe matamko ya kujijenga kisiasa, ni lazima tuwahurumie wasichana wanaokatishwa masomo kwa sababu ya mimba na kutafuta njia ya kuwanusuru lakini si kuwaongezea matatizo,” alisema.

Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Tandahimba, Sostenes Luhende alisema kuna kesi nyingi zimeripotiwa polisi za wanafunzi kupewa ujauzito lakini hakuna iliyopo mahakamani.

“Hakuna hata kesi moja ambayo tayari imefika mahakamani kwa maelezo tuliyopata polisi wanaendelea na uchunguzi,” alisema Luhende.

Alisema kinachochangia mimba kwa wanafunzi ni kuvunjika kwa ndoa kutokana na baadhi ya wazazi kushindwa kuvumiliana katika maisha, hivyo watoto kukosa malezi.

Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza, Michael Lugola alisema wanafunzi 33 wa shule za msingi mkoani Mwanza wamepata ujauzito, huku Wilaya ya Ukerewe ikiongoza kwa kuwa na matukio tisa, Magu ikifuata kwa mimba nane wakati halmashauri za Kwimba na Buchosa zikifungana kwa kuwa na matukio manne ya mimba.

Halmashauri za Misungwi, Ilemela, Nyamagana na Sengerema kila moja ina matukio mawili.

No comments

Powered by Blogger.