MAFURIKO YASOMBA NYUMBA 2,701 KILOSA

IDADI ya watu walioathiriwa na mafuriko
ya mvua katika kata 11 za vijiji 16 wilayani Kilosa, Morogoro,
imeongezeka kutoka kaya 1,831 zilizokuwa na watu 7,261 na kufikia kaya
2,701 zenye watu 9,345.
Aidha, mafuriko hayo yamesababisha
uharibifu wa miundombinu mbalimbali zikiwemo barabara na madaraja.
Mafuriko hayo yamesababisha pia kubomoka kwa nyumba 377 za makazi ya
watu katika maeneo ya vijiji hivyo na nyingine 2,266 kuzingirwa na maji
hayo.
Katika taarifa ya Kamati ya Maafa ya
Wilaya ya Kilosa iliyosomwa juzi na Katibu wa Kamati hiyo, Simfrosa
Mollel kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe, Mollel
alisema takwimu hizo ni za kuanzia tangu kutokea kwa athari za mafuriko
hayo Januari 8 hadi 12, mwaka huu.
Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua
zilizonyesha katika baadhi ya maeneo ya Kilosa na mikoa ya jirani,
ikiwamo Dodoma na Manyara na kusababisha maji kujaa Mto Mkondoa, kubomoa
sehemu ya kingo ya tuta na kuingia katika makazi ya watu na mashamba.
Alizitaja kata hizo zenye vijiji 16 kuwa
ni pamoja na Mkwatani, Chanzuri, Berega, Kidete, Magomeni, Masanze,
Mbumi, Tindiga, Mbigiri na Mabwerebwere. Mjumbe wa Kamati hiyo, Meja
Yenu Mgugule alimfahamisha Dk Kebwe kuwa, licha ya athari hizo, pia
nyumba 63 zimeezuliwa mapaa kutokana na upepo mkali uliotokea katika
vitongoji vya Vikwalaza na Tambuka Reli vilivyopo Kata ya Mikumi.
Alisema nyumba 53 ziliezuliwa na upepo
mkali katika Kitongoji cha Vikwalaza na nyingine10 katika Kitongoji cha
Tambuka Reli na kwamba, hakuna maafa zaidi yaliyoripotiwa kutokana na
nyumba hizo kuezuliwa.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Dk
Halima Mangiri alisema hawajapata taarifa yoyote kuhusu kutokea kwa
magonjwa ya mlipuko licha ya visima zaidi ya 13 vya maji ya kunywa
kuathiriwa na vingine kubomoka.
Dk Mangiri alisema hatua zilizochukuliwa
ni pamoja na usambazaji wa pakiti za dawa ya kutibu maji aina ya
“waterguard” zipatazo 15,810 zilizogawiwa katika kata zilizokumbwa na
athari hizo ili kutibu maji na kujikinga na magonjwa.
IMEANDIKWA NA JOHN NDITI,HABARILEO KILOSA
No comments