Ester Bulaya na Halima Mdee Wamaliza Kifungo Chao
Kifungo
walichokuwa wakitumikia wabunge wa Chadema, Ester Bulaya (Bunda Mjini)
na Halima Mdee (Kawe) cha kutokuhudhuria shughuli za Bunge kimemalizika
na wamesema wamerejea na kasi ileile.
Wabunge
hao waliadhibiwa kwa azimio la Bunge Juni 5 mwaka jana kutohudhuria
mikutano mitatu ya Bunge ambayo ni jumla ya siku 47, waliyokosa ukiondoa
shughuli zote za mikutano ya kamati za Bunge.
Adhabu
hiyo ilikwenda sanjari na kulipwa nusu mshahara na posho kwa kipindi
chote walichotumikia adhabu hiyo wakituhumiwa kudharau kiti cha spika.
Mikutano
mitatu waliyoikosa ni wa bajeti uliokuwa ukiendelea, wa saba
uliofanyika kati ya Septemba 5 hadi 15 na mkutano wa tisa wa Novemba 7
hadi 17.
Makato
ya mshahara na posho yamebainishwa katika Kanuni 75 ya Bunge inayosema:
“Mbunge aliyesimamishwa kazi atatoka katika Bunge na hataingia tena
katika sehemu yoyote ya ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge kwa muda wote
atakapokuwa amesimamishwa na atalipwa nusu mshahara na nusu posho
zinazoambatana na mshahara huo.”
Jana,
kwa nyakati tofauti Bulaya na Mdee walizungumzia kurejea kwao, huku
wakisema hawajutii kwa adhabu hiyo na hawatorudi nyuma au kutetereka
katika kusimamia wanachokiamini.
“Nitaendelea
kuwa Mdee yuleyule wa siku zote, kama walidhani wakinifungia mwaka
nitabadilika. Hapana! Sitaraji kubadilika. Nimetumwa na wananchi wangu
kusema ukweli na nitausema, sijaja kumpigia magoti mtu,” alisema.
Mdee
ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha),
alisema wakati akitumikia adhabu hiyo amepata fursa ya kufanya shughuli
kwa karibu za jimboni kwake na zile za Bawacha.
Naye Bulaya alisema: “Nimerudi bungeni tayari na leo (jana) nilihudhuria kamati yangu ya uwekezaji na mitaji.”
Alipoulizwa
amejifunza nini kutokana na adhabu hiyo, alisema: “Bulaya wa kukosoa,
Bulaya anayesimamia kile anachokiamini pasi na kuvunja sheria na
taratibu hajabadilika, nitaendelea kuwakosoa.”
“Hata
nilipokuwa natoka CCM kuja Chadema nilijua mambo kama haya ya
kukamatana, kufungiana yatakuwapo kwa hiyo nilijipanga na wala
hawanitetereshi, nimerudi na sitarudi nyuma,” aliongeza.
No comments