Header Ads

Barabara ya UKWAMA Makete yakamilika

 Muonekano wa Barabara hiyo baada ya kutengenezwa
 Mkandarasi wa barabara hiyo Bw. Asajile Mbwilo
 Diwani wa UKWAMA Mh Augustino Tweve
Mwananchi wa Ukwama Charles Sanga akizungumza na sisi
Hatimaye tatizo la kushindwa kupitika kwa barabara ya Ihobwela Hadi UKWAMA kata ya Ukwama wilayani Makete mkoani Njombe lililotokana na matengenezo ya barabara hiyo limemalizika baada ya mkandarasi kukamilisha kazi hiyo

Awali barabara hiyo ilipokuwa kwenye matengenezo ilipelekea adha kubwa kwa watumiaji ikiwemo kupanda kwa gharama za usafiri hasa bodaboda kutoka shilingi 4000 kwenda na kurudi hadi kufikia sh. 30,000 kwenda na kurudi

Blog hii imetembelea barabara hiyo kuanzia Ihobwela hadi Ukwama zikiwa zimepita wiki mbili tangu tutangaze kutopitika kwa barabara hiyo, na kukuta barabara hiyo inapitika kama awali baada ya mkandarasi kusambaza na kushindilia vifusi vilivyokuwepo barabarani hapo

Akizungumza nasi akiwa eneo la matengenezo ya barabara hiyo, Mkandarasi huyo Bw, Asajile Mbwilo amesema matengenezo ya barabara hiyo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 na barabara inapitika kama kawaida huku akiwapongeza Mkuu wa wilaya ya Makete Mh Veronica Kessy na mwenyekiti wa halmashauri Mh Egnatio Mtawa kufika kujionea hali ilivyokuwa awali kwenye barabara hiyo pamoja na Diwani wa kata ya Ukwama Mh. Augustino Tweve

Amesema kwa sasa kinachoendelea ni kufanya matengenezo ya kuzibua mitaro ili maji yapite na yasiharibu barabara pamoja na kuweka makalavati sehemu zinazohitajika kufanya hivyo

Pia amewaomba wananchi kuwa na uvumilivu wakati matengenezo ya barabara hiyo yanapofanyika kwa kuwa katika hatua za mwanzo za matengenezo hujitokeza changamoto mbalimbali ambazo kwa haraka wananchi hudhani hakuna kinachoendelea na kuanza kutoa lawama kumbe matengenezo yanaendelea na mwishowe ujenzi hukamilika

Diwani wa kata ya UKWAMA Mh. Augustino Tweve amesema tatizo lililokuwepo awali kwa sasa halipo kwa kuwa huduma zimerejea kama kawaida baada ya barabara hiyo kukamilika na kuiomba jamii kuliona na kulitambua hilo

Pia amewaomba wananchi kushirikiana naye kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuwa walimtuma kuwatumikia na yeye amehakikisha anawatumikia kama walivyomtuma na ndiyo maana ameshirikiana na viongozi mbalimbali wa halmashauri na mkandarasi kuhakikisha barabara hiyo inapitika kama kawaida

Baadhi ya wananchi waliozungumza na AM blog akiwemo Amasha, Charles Sanga na Agnes Ngailo wamempongeza mkandarasi, diwani wao na serikali kwa ujumla kwa kupambana kuhakikisha barabara hiyo inaendelea kupitika kama mwanzoni


Wamesema ni kweli walikuwa wakipata tabu mwanzoni wakati vifusi havijasambazwa, lakini sasa baada ya matengenezo kukamilika huduma zimerejea kama mwanzoni

No comments

Powered by Blogger.